Bondia wa Tanzania, Abdallah Pazi 'Dulla Mbabe', amesema haamini kama amepigwa na Eric Katompa na badala yake anaamini yeye ndiye mshindi katika pambano lililofanyika Jumamosi jijini Arusha.
Dulla amejikuta katika wakati mgumu baada ya kukubali kichapo kwa pointi kutoka kwa majaji watatu katika pambano la raundi 10 uzito wa 'Super Middle' lisilo la ubingwa.
Jaji wa kwanza alitoa alama 93-97, jaji wa pili alama 93-97 na jaji wa tatu alama 92-98.
Akizungumza na Pulsesports mara baada ya kumalizika kwa pambano hilo, Dulla amesema anaamini amepambana vizuri lakini haelewi kwanini hajapata matokeo ya ushindi.
"Mimi nimecheza vizuri kuanzia raundi ya kwanza hadi ya tatu na raundi zilizofuata tulikuwa tunabadilishana umiliki sasa sielewi imekuaje nimeshindwa," amehoji Dulla.
Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Dulla kupigwa na Katompa ambaye ni raia wa DR Congo, mara ya kwanza wawili hao walikutana mwaka 2021 ambapo Katompa alipata ushindi kwa pointi kama ilivyokuwa katika pambano hili la juzi usiku.
Kwa upande wa Katompa, amesema siri ya mafanikio yake dhidi ya mpinzani wake ni mazoezi makali ambayo huwa anafanya wakati wa maandalizi.
Aidha amebainisha Dulla hajabadilika chochote katika mbinu zake tangu mara ya mwisho walipokutana.