Bondia wa ngumi za kulipwa nchini Tanzania uzito wa juu mwepesi, Twaha Kiduku, amesema kama bondia Hassan Mwakinyo yupo tayari basi wakutane ulingoni.
Kiduku ametoa majibu hayo ikiwa ni kwa mara ya kwanza tangu Mwakinyo alipoanza kumrushia vijembe mwezi uliopita wakati akitangaza pambano lake.
Akizungumza na Pulsesports kwa simu akiwa mkoani Morogoro, Kiduku amesema anajua fika kwamba Mwakinyo anamuogopa na ndio maana anakwepa kupigana naye ila kwasasa kama yupo tayari basi wasaini mkataba.
"Mimi sio mtu wa kuongea sana na sina fani hiyo, najua jamaa ananiogopa na ndio maana ananikwepa ila kwasasa kama yupo tayari basi tupigane tumalize ubishi," amesisitiza.
Kauli ya Kiduku inatarajiwa kuongeza chachu kuelekea kuandaliwa kwa pambano hilo la ngumi ambalo wadau wengi wa masumbwi wamekuwa wakiliota kutokea.
Mwishoni mwa wiki hii, Mwakinyo amenukuliwa akisema yupo tayari kupigana na bondia yeyote kutoka Tanzania kama watatokea watu wakuandaa pambano.
Hayo amesema mara baada ya kufanikiwa kushinda mkanda wa WBO Afrika, kwa kumtwanga Mghana, Elvis Ahorgah kwa TKO raundi ya saba.