Kamisheni ya Kusimamia Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC), imemfutia adhabu ya kumfungia mwaka mmoja bondia, Hassan Mwakinyo.
Mbali na kufuta adhabu ya kifungo lakini pia wamemfutia faini ya sh. milioni 1 ambayo ilikuwa ni sehemu ya adhabu hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jijini Dar es Salaam na Ofisa Habari wa TPBRC, Lugano Israel, wamefikia uamuzi huo baada ya bondia huyo kukiri makosa yake na kuomba radhi.
"Baada ya kukutana mara kadhaa na Mwakinyo, amekiri makosa yake na ameahidi kutorudia tena hivyo sisi kama walezi tumeona bora tumsamehe," amesema Israel.
Mwakinyo alifungiwa kupanda ulingoni kwa kipindi hicho kutokana na kosa la kushindwa kupanda ulingoni kwa makusudi katika pambano lake dhidi ya Julius Indongo, lililotakiwa lifanyike Septemba 29, mwaka huu.
Adhabu dhidi yake ilitolewa na kamisheni hiyo Oktoba 10 na kwa maana hiyo ameitumika adhabu kwa kipindi ambacho hakijafika miezi miwili tangu afungiwe.