Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), limeipa nchi ya Tanzania video za usaidizi wa marefa (VAR) ambazo zitafungwa nchini kwenye viwanja vyenye ubora.
Hayo yamethibitishwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia wakati akitoa hotuba yake kwenye Mkutano Mkuu wa Shirikisho hilo uliofanyika mkoani Iringa.
Karia amesema tayari wataalamu wa kufunga vifaa hivyo na kutoa mafunzo wameshafika nchini tangu jana na kazi itaanza hivi karibuni.
Aidha amesema kupewa vifaa hivyo ni kutokana na ushirikiano mzuri kati yao na CAF.
"Hivi karibuni tutaanza zoezi la kufunga VAR, wataalamu wameshafika tangu jana," amesema.
Zoezi hilo linatarajia kufanyika katika viwanja ambavyo vimekizi vigezo vya CAF ikiwemo Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.
Tanzania ikifanikiwa kufunga VAR itaungana na nchi zingine za Afrika kama Misri, Algeria na Morocco ambazo tayari zinatumia kifaa hicho.