Kiduku amuonya Kidunda atakapopanda ulingoni kumvaa Wellem
Bondia wa Kulipwa nchini Tanzania, Twaha Kiduku, amemuonya bondia mwenzake, Seleman Kidunda ambaye wiki ijayo atacheza pambano lake dhidi ya Asemahle Wellem.
Kiduku ambaye ameshawahi kupigana na Wellem mwaka jana, amemwambia Kidunda kuwa asimchukulie poa bondia huyo kwani anaweza kumshtukiza kama ilivyotokea kwake.
Akizungumza na Pulsesports, Kiduku amesema Wellem ni bondia mchanga ambaye anatafuta jina lake katika anga la masumbwi Afrika hivyo anajitahada ambazo wakati mwengine ni changamoto kwa wapinzani hasa wenye majina kama Kidunda.
"Ninachompa ushauri ni kwamba asimchukulie poa, apigane naye mwanzo mwisho bila kuzubaa ulingoni kwani inaweza kumletea shida," amesema.
Kiduku alipigana na Wellem Julai, mwaka jana katika pambano la raundi 10 ambalo lilichezwa Ubungo Plaza, Dar es salaam na mwenyeji alipoteza kwa pointi za majaji wote watatu.
Wellem atapanda tena ulingoni Machi Mosi kuzichapa na Kidunda katika pambano lisilo la ubingwa la raundi 12 ambalo litafanyika katika Ukumbi wa Warehouse, Dar es Salaam.
Kidunda na Wellen watapanda ulingoni kuwania mkanda wa Dunia wa WBF katika pambano lililopewa jina 'Usiku wa Vita'.
Mbali na pambano hilo kuu, litatanguliwa na pambano kati ya bondia Mtanzania, Loren Japhet ambaye atazichapa na Mzambia Hillary Kataya.
Pambano lingine ni kati ya bondia, Nassibu Ramadhani ambaye atazichapa na Mnamibia, Immanuel Naidjala.