Kocha Simba ajivunia kupata kikosi cha kwanza
Kocha wa Makipa wa timu ya Simba SC, Daniel Cadena, amesema kwasasa timu hiyo imeshapata kikosi chake cha kwanza na hatarajii kuona mabadiliko makubwa ya mara kwa mara.
Akizungumza jijini Mwanza, Cadena amesema awali benchi la ufundi chini ya Kocha, Abdelhak Benchikha ambaye ni mgeni ndani ya timu walikuwa wakijaribu kutafuta uwiano wa kikosi kulingana na wachezaji waliokuwepo kitu ambacho anasema kwasasa kimetimia.
Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumzia maandalizi kuelekea mchezo wa kesho wa Ligi Kuu Bara ambapo Simba itacheza dhidi ya Geita Gold katika Uwanja wa CCM Kirumba.
"Kwasasa tunao wachezaji wazuri 11 kuanzia golini na wachezaji wa ndani ambao wanatarajia kuanza mara kwa mara katika michezo yetu mbalimbali, hii haikuwa hivi mwanzoni wakati tunaanza kazi," amesema.
Katika kikosi ambacho kimecheza mechi nyingi za hivi karibuni tangu kurejea kwa ligi hasa kwa wachezaji wapya Ayoub Lakred, Babacar Sarr, Pa Omar Jobe na Freddy Michael wanaonekana kupata nafasi za kucheza mara kwa mara.
Aidha wachezaji kama Israel Mwenda, Hussein Kazi, Edwin Balua, Saleh Karabaka wameonekana wakitumika mara kwa mara hata kwa kuingia wakiwa wanatokea benchi.
Wachezaji wa zamani ambao nafasi zao zinaonekana kuwa hatarini kupotea kwenye kikosi cha kwanza ni pamoja na Kipa, Aishi Manula, Mzamiru Yassin, Shomari Kapombe na Sadio Kanoute.
Saido Ntibanzokiza, Clotus Chama, Mohamed Hussein, Che Malone ni wachezaji ambao bado wanaonekana kuwa katika mipango ya kikosi cha kwanza hasa ukiangalia aina ya vikosi vilivyopangwa katika mechi za karibuni.
Simba itacheza mchezo wao wa nne ndani ya siku 10 ikiwa ni ratiba yao ya mechi za viporo ambayo waliianza tangu Februri 3 ligi iliporejea.