Bondia wa ngumi za kulipwa nchini Tanzania, Hassan Mwakinyo, amesema anajivunia kushinda tuzo yake ya kwanza ndani ya mipaka ya nchi.
Mwakinyo ametangazwa kuwa Mwanamichezo Bora wa Januari, 2024 wa tuzo za Chama cha Waandishi wa Habari wa Michezo Tanzania (TASWA) katika hafla ya uzinduzi wa tuzo hizo zilizofanyika Msasani Beach Club, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki na kuhudhuriwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia, Nape Nnauye.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Mwakinyo amesema kwa miaka mingi amekuwa katika tasnia ya masumbwi lakini zaidi ya mikanda ambayo mara kadhaa amekuwa akishinda uliongoni hajawahi kupata tuzo ya kutambua uwezo wake nje ya ulingo.
Amesema tuzo hiyo ni ya kwanza kwake na yeye anajivunia kuwa mwanamichezo bora wa mwezi Januari mwaka huu kwani itamuongezea chachu ya kuendelea kufanya vyema zaidi ili kufanya mambo makubwa zaidi.
"Hakika bila kuwa muongo hii ndio tuzo yangu ya kwanza kuipata nje ya ulingo, ninajivunia kwa mafanikio haya na nina washukuru waandaaji kwa kutambua mchango wangu," amesema.
Mwakinyo amefikia mafanikio hayo baada ya mwishoni mwa mwezi uliopita kuibuka na ushindi wa TKO raundi ya saba dhidi ya bondia Mghana, Elvis Ahorgah na kushinda mkanda wa WBO Afrika.
Katika hatua nyingine, Mwakinyo ameeleza mipango yake ya hivi karibuni ambapo anatarajia kupigana katika pambano la ubingwa ndani ya miezi mitatu ijayo.
Amesema kwa mujibu wa mkanda wa WBO Afrika alioshinda hivi karibuni, ana siku zisizopungua 120 na zisizozidi 150 kutetea mkanda huo ulingoni.
Tuzo za TASWA zimezinduliwa rasmi na sasa kila mwezi watakuwa wakimtangaza mwanamichezo bora kabla ya kuja kumtaja mwanamichezo bora mwisho wa kila mwaka.