Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameipongeza timu ya Taifa ya Soka Wanawake ‘Twiga Stars' kwa kuwapa sh. milioni 200 kama motisha baada ya kufuzu kwenye michuano ya WAFCON ambayo inatarajia kufanyika mwakani nchini Morocco.
Twiga imefikia mafanikio hayo baada ya kuwaondosha Togo kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya mechi mbili zilizofanyika kwa mtindo wa nyumbani na ugenini.
Akifikisha salamu hizo, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro ambaye amekuwepo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuipokea timu hiyo, amesema serikali inajivunia mafanikio ya kikosi hicho cha Twiga Stars.
Amesema Rais Samia amevutiwa na mafanikio hayo na amewapa fedha hizo ikiwa ni sehemu yake ya hamasa zake katika kuunga mkono sekta ya michezo.
‘Rais Samia amefurahishwa sana na mafanikio yenu na ndio maana ametoa kiasi cha shilingi milioni 200 ili kuwapa pongezi zake kwenu,’ amesema Ndumbaro.
Waziri Ndumaro ameongeza kwa kusema nchi ya Tanzania kwasasa imepiga hatua katika anga la michezo na hii ikiwa ni kwa mara kwanza timu zote za taifa za wakubwa kushiriki michuano hiyo mikubwa kwa wakati mmoja.
Ikumbukwe kuwa timu ya Taifa ya Wanaume 'Taifa Stars' nayo imefuzu kwenye michuano ya Afcon ambayo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi nchini Ivory Coast mwezi ujao.
Hii ni mara ya pili kwa Twiga Stars kucheza WAFCON, mara ya kwanza walifanya hivyo mwaka 2010.
Michuano hiyo inashirikisha timu 12 na katika Ukanda wa CECAFA ni Tanzania pekee ndio wamekata tiketi. Timu zingine ambazo zimefuzu ni wenyeji Morocco, Algeria, Botswana, DR Congo, Ghana, Mali, Nigeria, Senegal, Afrika Kusini, Tunisia na Zambia.