Advertisement
KANDANDA

Simba SC yatamba kushusha 'vifaa' vipya dirisha dogo

Klabu hiyo imeonekana kupungua makali msimu huu na ndio maana inataka kufanya usajili ili kuongeza nguvu katika kikosi chao
Advertisement

Uongozi wa Klabu ya Simba, umeweka wazi katika dirisha hili la usajili wamedhamiria kufanya kweli ili kuirejesha timu katika makali yake ya kuwania mataji.

Advertisement

Hayo yamebainishwa na Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, ambaye amesema usajili wa dirisha hilo utakuwa ni kubwa kuliko.

Ally amesema katika kipindi hiki cha mapumziko ya mwisho wa mwaka wao kama viongozi hawajapumzika badala yake wapo makini kuhakikisha furaha inarejea kwa mashabiki na wanachama wa klabu hiyo.

Amesema wamepokea mapendekezo ya Kocha, Abdelhak Benchikha kuhusu maingizo mapya na tayari kazi imeshaanza kufanyika ili kuhakikisha kuwa wao hawawi sehemu ya kukwamisha mipango ya ushindi.

"Ukifuatilia unaweza kuona kama tupo kimya lakini sio kweli, tupo makini kweli tukifanya mambo mbalimbali ya kunasa wachezaji kama tulivyoagizwa na benchi la ufundi, kwa kifupi furaha ya wana Simba inaandaliwa nyuma ya pazia," amesema.

Advertisement

Katika dirisha hilo, Simba wanahusishwa na baadhi ya nyota wa ndani na nje ya nchi ambapo pia baadhi ya wachezaji wanatajwa kuwa watapewa mkono wa kwaheri.

Hadi sasa licha ya ukimya uliopo lakini inaelezwa kuwa winga chipukizi wa timu ya Mtibwa Sugar, Ladack Chasambi, ameshamwaga wino wa kuitumikia timu hiyo.

Mbali na Chasambi lakini pia kumekuwa na majina mengine mengi yakihusishwa na timu hiyo hasa kutoka nje ya nchi wakiwemo Erick Mbangossoum (Chad) na Mauricio Cortes (Colombia).

Pia klabu hiyo inatarajia kupunguza baadhi ya nyota ambao wanaonekana kushindwa kuendana na timu akiwemo Aubin Kramo ambaye alisajiliwa mwanzo wa msimu akitokea Asec Mimosa, pia mchezaji kama Moses Phiri taarifa zinadai kuwa ameomba kuachwa.

Kuhusu michuano ya Mapinduzi Cup, Ally amesema wanatarajia kushiriki na kikosi chao kamili cha wachezaji wote ambao hawapo katika timu za taifa.

Advertisement

Simba waliingia kambini tangu Jumatano na wanatarajia kuanza kucheza mechi yao ya kwanza katika michuano hiyo Januari Mosi dhidi ya JKU.

Advertisement
Advertisement
More from Pulse Sports Uganda