Timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania 'Twiga Stars', imetinga raundi ya tatu ya michuano ya kufuzu Michezo ya Olimpiki mwakani jijini Paris, Ufaransa kwa kuitoa Botswana kwa jumla ya mabao 3-0.
Ushindi huo sasa unaifanya Twiga Stars kukutana na Afrika Kusini 'Banyana Banyana' ambayo iliitoa DR Congo katika raundi ya pili kufuzu Olimpiki ya Paris 2024.
Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, Twiga Stars ilishinda mabao 2-0, mabao yao walifungwa na Aisha Masaka na Oppa Clement.
Mchezo wa marudiano uliopigwa usiku wa kuamkia Novemba Mosi nchini Botswana, Twiga Stars iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Masaka ambaye anacheza soka la kulipwa nchini Sweden katika Klabu ya Daraja la Kwanza ya BK Hacken.
Baada ya mchezo huo kumalizika, Kocha wa timu ya 'Twiga Stars', Bakari Shime, amesema haukuwa mchezo mwepesi kwani wapinzani wao walikuwa wakihitaji matokeo ili kusonga mbele.
"Tunashukuru tumepata matokeo mazuri na kusonga mbele hatua ya raundi ya tatu na sasa tutakutana na Afrika Kusini, ambayo itakuwa ni timu bora zaidi ya wapinzani wetu waliopita" amesema Shime.
Amewapongeza wachezaji wake kwa kupambana na kuitoa Botswana kwani haikuwa timu nyepesi kutokana na kutumia mfumo wa kupiga mipira mirefu.
Pia amezungumzia mwishoni mwa mwezi huu watakuwa na mchezo wa kufuzu WAFCON 2024 dhidi ya Togo na marudiano yatakuwa Novemba 5.
Hivyo kutokana na ratiba hiyo kwa sasa wachezaji wao watarejea katika klabu zao kabla ya kuanza kujiandaa na michezo hiyo.