Advertisement
Ligi Kuu

Yanga SC yajikita kileleni ikiichapa Prisons 2-1

Pia Mfadhili wao, Ghalib Said Mohamed 'GSM' amekubali kujenga uwanja Jangwani
Advertisement

Timu ya Yanga SC, imeendelea kujichimbia kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kuitandika Tanzania Prisons mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Advertisement

Ushindi huo, umeifanya Yanga kufikisha alama 40 na kumalizika mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo kwa kishindo huku Prisons ikibaki nafasi ya tisa kwa alama 17.

Pia ushindi huo pia umenogesha 'birthday' ya timu hiyo ambayo leo ilikuwa ikisherehekea kutimiza miaka 89 tangu kuanzishwa kwake.

Pamoja na shangwe hizo za Yanga, ilimaliza ikiwa pungufu baada ya Kipa wao, Metacha Mnata kuoneshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja na Mwamuzi, Ahmed Arajiga baada ya kumchezea vibaya Jeremiah Juma huku pia mchezaji Zabron Mayombya alioneshwa kadi ya pili ya njano na kuwa nyekundu baada ya kujiungusha ndani ya eneo la hatari.

Katika mchezo huo ambao kabla ya kuanza, viongozi wa timu hiyo walikata keki uwanjani ya kutimiza miaka 89 lakini pia kulikuwa na dakika moja ya kusimama kumuombea aliyekuwa Mwenyekiti wa timu ya Yanga, Iman Madega ambaye alifariki Jumamosi na kuzikwa leo.

Advertisement

Mabao ya Yanga katika mchezo huo, yalifungwa na Clement Mzize pamoja na Pacome Zouazoua huku la kufutia machozi kwa Prisons likifungwa na Jeremiah Juma kwa mpira wa adhabu ndogo uliokwenda moja kwa moja wavuni.

Mchezo huo ulikuwa na ushindani wa aina yake kutokana na uwanja kutokuwa rafiki kwani pamoja na Yanga kucheza pasi za chini chini lakini walipata changamoto katika umaliziaji.

Prisons yenyewe ilikuwa ikiwasubiri Yanga nyuma lakini ilikuwa ikifanya mashambulizi ya kushtukiza kwa kutumia mipira mirefu.

Kabla ya mchezo, timu ya Tabora United, imelazimishwa sare ya bao 1-1 na Namungo FC katika mfululizo wa mechi za ligi hiyo.

Wenyeji Tabora ilikuwa ya kwanza kufunga bao kupitia kwa Erick Okotu dakika ya 11 kabla ya Pius Buswita kusawazisha dakika ya 37.

Advertisement

Matokeo hayo, yameifanya Tabora Utd kufikisha kufikisha alama 16 ikiwa nafasi ya 12 huku Namungo ikifikisha alama 18 katika nafasi ya saba.

Katika hatua nyingine, Mfadhili wa klabu hiyo, Ghalib Said Mohamed 'GSM', ameridhia ombi la kujenga uwanja kwa ajili ya timu hiyo.

Advertisement
Advertisement
More from Pulse Sports Uganda