Onana aifungia Simba SC mabao 2 ikiichapa Wydad Casablanca

KANDANDA Onana aifungia Simba SC mabao 2 ikiichapa Wydad Casablanca

Na Zahoro Mlanzi • 18:42 - 19.12.2023

Ushindi huo, umefufua matumaini ya timu hiyo katika kuwania nafasi ya kucheza robo fainali ya michuano hiyo

Straika wa kimataifa wa Cameroon, Willy Onana, ameifungia mabao mawili timu yake ya Simba SC na kuiwezesha kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Wydad Casablanca, katika mfululizo wa mechi za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Onana ambaye katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, amecheza nyuma ya mshambuliaji, Jean Baleke bada ya kutokea winga wa kushoto kama ilivyozoeleka.

Ushindi huo, umefufua matumaini ya Simba kucheza hatua ya robo fainali ya michuano hiyo kwani imefikisha alama 5 nyuma ya vibara Asec Mimosa yenye alama 7.

Hata hivyo, Asec Mimosa baadaye itakuwa uwanjani kuumana na Jwaneng Galaxy yenye alama 4 katika kundi hilo la B.

Onana alifunga bao la kwanza dakika ya 36, kwa shuti kali nje ya eneo la hatari baada ya kupokea pasi ya Kibu Denis na mpira kujaa wavuni.

Kabla ya mashabiki wa Simba, hawajapoa kwa furaha, Onana tena alirejea kambani dakika ya 38 safari hii akipokea pasi safi kutoka kwa Mzamiru Yassin. Mabao hayo yalidumu hadi mapumziko.

Pamoja na matokeo hayo, mashabiki wa Simba hawatosita kumpongeza Kipa wao, Ayoub Lakred ambaye aliokoa nafasi tatu za wazi.

Kipindi cha pili, kilianza kwa Wydad kuwa na nguvu na kwa wakati fulani waliwadhibiti Simba kwa muda mrefu langoni mwao.

Hata hivyo, ukuta wa Simba chini ya Henock Inonga na Che Malone Fondoh, ulionekana kuwa imara kuondosha hatari zote hasa za mipira ya juu.

Straika wa Simba, Jean Baleke, alikosa nafasi ya wazi kuandika bao la tatu baada ya kuunganisha vibaya pasi ya chini iliyopigwa na Shomari Kapombe.

Katika mchezo huo, Benchikha aliwapa nafasi ya kuingia kipindi cha pili wachezaji John Bocco, Kennedy Juma, Israel Mwenda, David Kameta 'Duchu' na Abdallah Khamis.

Huu ni ushindi wa kwanza kwa Simba kwenye michuano ya kimataifa msimu huu baada ya kushindwa kufanya hivyo katika michezo mitano iliyopita.

Baada ya mchezo huo, michuano hiyo sasa itasimama kwa muda kupisha michuano ya Afcon ambayo inatarajiwa kuanza mwezi ujao.

Kikosi cha Simba kwasasa kitaelekeza nguvu zake kwenye mechi za Ligi Kuu ambapo mwisho wa wiki watakabiliana na Tabora United.