Simba SC yaingia kambini kuiwinda Kagera Sugar

KANDANDA Simba SC yaingia kambini kuiwinda Kagera Sugar

Zahoro Mlanzi • 11:00 - 13.12.2023

Inaingia kambini ikitoka kufungwa bao 1-0 na Wydad Casablanca katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika

Kikosi timu ya Simba SC, kimeingia kambini leo kujiandaa na maandalizi kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar, unaotarajia kupigwa Ijumaa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Simba imerejea nchini Jumatatu ikitokea Morocco ambapo walicheza na Wydad na kupoteza kwa bao 1-0 kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika Ligi Kuu Bara, Simba ipo nafasi ya nne ikiwa na alama 19 baada ya kushuka dimbani katika michezo 8.

Huu utakuwa ni mchezo wa kwanza wa ligi kwa Benchikha ambaye tangu amechukuwa timu hiyo ameiongoza kwenye mechi mbili za kimataifa.

Akizungumza na Pulsesports, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema kwasasa wachezaji wanaanza kurejea kambini kwa ajili ya michezo inayofuata wakianza na huo wa Ijumaa dhidi ya Kagera Sugar.

"Timu ilikuwa na mapumziko mafupi baada ya mechi ngumu ya ugenini, kikosi kinarejea kambini kuanzia leo na baada ya hapo maandalizi yanaendelea," amesema.

Mara baada ya Simba kucheza na Kagera Sugar, itakuwa na mchezo mwingine muhimu Jumanne ambapo watawakaribisha Wydad Casablanca Uwanja wa Mkapa, Dar es Saalam.

Mchezo huo utakuwa ni kama wa kutaka kulipa kisasi kutokana na Simba kukubali kichapo katika mechi iliyopita mwisho wa wiki cha bao 1-0.

Mbali na mechi hizo mbili lakini ndani ya mwezi huu, Simba itakuwa na mechi nyingine tatu za Ligi Kuu ambazo ni dhidi ya KMC, Mashujaa FC na Tabora United ambazo zote watakuwa ugenini.