Gamondi alia na mwamuzi kuwanyonya dhidi ya Medeama

KANDANDA Gamondi alia na mwamuzi kuwanyonya dhidi ya Medeama

Zahoro Mlanzi • 16:36 - 09.12.2023

Kocha huyo wa Yanga anadai mwamuzi huyo kutoka Libya hakuwa anatoa maamuzi sahihi

Kocha wa timu ya Yanga SC, Miguel Gamondi, amemtupia lawama mwamuzi wa kati wa mchezo baina ya timu yake dhidi ya Medeama ambao ulimalizika kwa sare ya 1-1.

Mchezo huo wa mzunguko wa tatu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika ulichezwa nchini Ghana katika Uwanja wa Baba Yara jana usiku.

Mabao katika mchezo huo, yamefungwa na Jonathan Sowah kipindi cha kwanza kwa mkwaju wa penalti na kisha Pacome Zouzoua akasawazisha kwenye kipindi hicho.

Mara baada ya mchezo huo, Kocha Gamondi amemtupia lawama Mwamuzi, Mutaz Ibrahim kutoka Libya kwa kitendo cha kuwazawadia wenyeji penalti ambayo anadai kuwa haikustahili.

Mbali na tukio la penalti lakini pia Gamondi amekumbushia tukio la mchezaji wake, Nickson Kibabage kuchezewa faulo mbaya lakini mwamuzi alishindwa kutoa uamuzi sahihi kwa kumpa kadi ya njano Kwadwo Asamoako.

"Mwamuzi wa mchezo wa leo (jana) ametumaliza kabisa, kwa mtazamo wangu ile haikuwa penalti lakini pia mchezaji wa Medeama alitakiwa kutolewa nje kutokana na faulo mbaya aliyocheza," amesema Gamondi.

Matokeo ya mchezo huo, yanawaacha Yanga wakiwa mkiani katika Kundi D wakiwa na alama 2 baada ya kushuka dimbani mara tatu.

Vinara wa kundi ni Al Ahly wenye alama 5 baada ya wao pia kulazimishwa suluhu nyumbani na CR Beluizdad katika mchezo mwengine wa kundi hilo.

Beluizdad wao wapo katika nafasi ya pili wakiwa na alama 4 sawa na Medeama ambao wapo nafasi ya 3.

Mechi za mzunguko wa nne zinatarajia kupigwa Desemba 20 ambapo Yanga watakuwa ni wenyeji wa Medeama huku CR Beluizdad wakiwakaribisha Al Ahly.