Gamondi asuka upya safu ya ulinzi kuivaa Medeama SC

KANDANDA Gamondi asuka upya safu ya ulinzi kuivaa Medeama SC

Na Zahoro Mlanzi • 14:34 - 07.12.2023

Kocha huyo wa Yanga, Ijumaa ataiongoza timu yake ugenini kusaka alama 3 za kwanza katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika

Kuelekea mechi yao ya kesho dhidi ya Medeama SC ya Ghana, Kocha wa timu ya Yanga SC, Miguel Gamondi, ameonekana kufanyia kazi zaidi eneo lake la ulinzi ili kutoruhusu mabao mengi.

Timu hiyo imeshatua mjini Kumasi nchini Ghana na kufanya mazoezi ikijindaa na mchezo huo utakaopigwa kuanzia saa 1 usiku kwa saa za Afrika Mashariki na Kati.

Kwa mujibu wa taarifa iliyowekwa katika mtandao wa kijamii wa X wa klabu hiyo, Gamondi ameweka wazi atafanyia kazi kwa kiasi kikubwa katika ulinzi hususani katika michuano hiyo.

Katika mechi mbili ilizoshuka uwanjani hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, ukuta wa Yanga uliokota mabao manne, ugenini dhidi ya CR Beloizdad ilitunguliwa mabao matatu na Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam dhidi ya Al Ahly ilifungwa bao moja.

Gamondi amesema makosa waliyofanya kwenye mechi za kimataifa ni sehemu ya mchezo jambo ambalo linafanyiwa kazi katika uwanja wa mazoezi.

“Utaona kwamba mabao ambayo tulifungwa ilitokana na namna ya kuzuia makosa ambayo tulifanya. Hapo ni muhimu kwetu kuangalia namna ya kurejea katika ubora na sehemu ya mazoezi tunafanyia kazi hayo," amesema.

"Kikubwa ni kuona kwamba hatufanya makosa mengi kwenye eneo letu la hatari kwani wapinzani nao wanatafuta matokeo, hivyo hilo tunalifanyia kazi kwa ajili ya kuwa imara kwa mechi zijazo.” ameongeza.

Safu ya ulinzi ya Yanga inayotarajiwa kuvaana na Medeama, itaongozwa na Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Bacca.

Hadi sasa mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara, inashika mkia Kundi D ikiwa na alama 1 huku Al Ahly ikiongoza ikiwa na alama 4 ikifuatiwa na Medeama na Belouzdad zenye alama 3 kila mmoja.

Tags: