Msuva akubali kuvunja mkataba na JS Kabylie ya Algeria

KANDANDA Msuva akubali kuvunja mkataba na JS Kabylie ya Algeria

Zahoro Mlanzi • 16:03 - 20.12.2023

Uamuzi huo umefikiwa baada ya klabu hiyo kuomba kufanya hivyo kutokana na kutoridhishwa na kiwango chake

Winga wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Simon Msuva, kwasasa ni mchezaji huru baada ya kuachana na Klabu yake ya JS Kabylie inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini Algeria.

Msuva alijiunga na timu hiyo mwanzoni mwa msimu huu na amehudumu hapo kwa kipindi kisichozidi miezi sita.

Timu ya JS Kabylie inashika nafasi ya tisa kwenye Ligi ya Algeria baada ya kucheza michezo 10 na kukusanya alama 14.

Kabla ya kujiunga na timu hiyo, Msuva alikuwa akicheza timu ya Al Qadsiah FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini Saudi Arabia.

Akiwa ndani ya timu hiyo, amefanikiwa kucheza mechi sita za ushindani na hajawahi kufunga bao lolote.

Msuva alijiunga na timu hiyo ikiwa ni pendekezo la Kocha, Youcef Bouzidi lakini kocha huyo hakudumu kikosini hapo baada ya kutimuliwa kazi mapema Oktoba na nafasi yake kuchukuliwa na Rui Almeida. Tangu alipoingia kocha huyo raia wa Ureno, nafasi ya Msuva kwenye kikosi cha kwanza ikawa ni ya kususua.

Taarifa ya klabu ambayo ilitolewa katika kurasa rasmi, ilieleza kufikia makubaliano ya pande mbili kuvunja mkataba wa Msuva na hivyo walimtakia kila la kheri kwenye maisha yake mengine ya soka.

"Tumekubaliana kuvunja mkataba wa Simon Msuva, tunamtakia kila la kheri huko aendapo," ilisomeka taarifa ya klabu hiyo.

Kuelekea dirisha la usajili la Januari nchini Tanzania, kuna uwezekano wa Msuva kuhusishwa na baadhi ya timu ambazo zitahitaji huduma yake.

Ikumbukwe kuwa kabla hajaanza maisha yake ya soka nje ya nchi, Msuva amewahi kutamba na timu za Moro United na Yanga SC.

Kabla ya kwenda Algeria, timu za Simba na Yanga, zilikuwa zikihitaji huduma yake ila walishindwana katika ada ya uhamisho.