Simba SC yazindua kampeni maalum kuifunga Wydad

KANDANDA Simba SC yazindua kampeni maalum kuifunga Wydad

Zahoro Mlanzi • 05:30 - 15.12.2023

Timu hiyo hadi sasa inashika mkia Kundi B la michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa na alama 2

Klabu ya Simba, imeweka wazi mipango yake kuelekea mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad Casablanca ambapo wanataka kuutumia mchezo huo kuwa njia ya kuelekea robo fainali huku wakizindua kauli mbinu yao ya 'Haijaisha hadi iishe'.

Mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa unatarajia kuchezwa Jumanne kuanzia saa 10 jioni katika Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema katika mchezo huo wao kama uongozi hawahitaji chochote zaidi ya ushindi ili kufufua matumaini yao ya kusonga mbele kutoka kwenye hatua ya makundi.

Amesema msimu huu walikuwa na lengo la kufika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo na hivyo ili kufanikisha hilo wanapaswa kuwafunga Wydad ili kupata ushindi wao wa kwanza wa hatua ya makundi msimu huu.

"Msimu huu tulijiwekea lengo la kucheza nusu fainali kwahiyo itakuwa ni aibu kubwa kama tutashindwa kuvuka katika kundi hili," amesema.

Katika kuhakikisha hamasa ya mchezo huo inakuwa kubwa, uongozi wa Simba wamemtambulisha DJ maarufu kwenye mitandao ya kijamii, Miso Misondo kuwa atakuwepo uwanjani siku hiyo huku Kocha, Abdelhak Benchikha akitajwa kuwa ni mgeni rasmi wa mchezo huo.

Kiingilio wa mchezo huo cha chini sh. 5,000 kwa viti vya mzunguko, VIP C ni sh. 10,000, VIP B ni sh. 20,000, VIP A ni sh. 30,000 na Platinum ni sh. 150,000.

Simba ipo mkiani katika Kundi B la michuano hiyo baada ya kuvuna alama 2 katika mechi tatu za awali wakiwa wamefungwa mchezo mmoja na kwenda sare michezo miwili.

Katika hatua nyingine, timu hiyo kesho itashuka Uwanja wa Uhuru kuumana na Kagera Sugar katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara huku Kocha, Benchikha akisema wanachohitaji ni ushindi katika mchezo huo.

"Nafurahi kuanza kucheza michezo ya ligi ndani ya Tanzania, siku zote mechi za ligi huwa ni ngumu lakini sisi malengo yetu ni kufanya vizuri kwenye mechi zote," amesema.

Kwa upande wa Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Mexime, amesema wanakwenda kucheza mchezo mgumu dhidi ya timu ambayo imejikusanyia uzoefu wa kutosha kwenye michezo ya kimataifa