Yanga SC, Simba SC kuvuna 'goli la Mama' kivingine

KANDANDA Yanga SC, Simba SC kuvuna 'goli la Mama' kivingine

Zahoro Mlanzi • 20:37 - 12.12.2023

Huo ni utaratibu ambao umekuwa ukifanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa sh. milioni 5 kwa kila bao litakalofungwa na timu hizo kimataifa

Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amesema utaratibu wa kutoa fedha za 'goli la mama' bado unaendelea ingawa kwasasa kuna mabadiliko kidogo na ndio maana hadi sasa hakuna timu ambayo imepata zawadi hiyo.

Msimu uliopita kuanzia katika hatua ya makundi, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliahidi kutoa kiasi cha shilingi milioni tano kwa timu ambazo zilikuwa zinashiriki katika hatua ya makundi ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika ambazo ni Simba na Yanga.

Utaratibu huo umeonekana kuongeza hamasa kwa timu hizo ambazo kwa nyakati tofauti zilifanya vizuri na kusababisha Yanga kufika hadi hatua ya fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho.

Hata hivyo, msimu huu licha ya timu zote kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na tayari zimeshacheza mechi tatu lakini kumekuwa na ukimya kuhusu zawadi hizo huku wengine wakidhani kuwa huenda ahadi hiyo imefutwa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Msigwa amesema ahadi ya shilingi milioni 5 kwa kila bao bado ipo pale pale isipokuwa kwasasa timu inatakiwa kuibuka na ushindi ili kutimiza vigezo vya kupata fedha hizo.

"Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameona ni vyema tuhamasishe zaidi timu ishinde ndio tutoe fedha, kwa mwaka huu hadi sasa hakuna timu ambayo imeshinda na ndio maana umeona hatujatoa fedha yoyote," amesema Msigwa.

Ameongeza kwa kusema anaamini katika michezo inayofuata ya timu hizo zitaibuka na ushindi na kujizolea fedha hizo.

Aidha Msigwa amewataka mashabiki wa soka nchini kuwa na uzalendo na timu zao pamoja na taifa badala ya kufanya fujo au kuzomea wachezaji pindi matokeo yanapokuwa hayapo upande wao.