Wachezaji Simba SC wawekwa kiti moto matokeo mabaya

KANDANDA Wachezaji Simba SC wawekwa kiti moto matokeo mabaya

Zahoro Mlanzi • 21:08 - 27.11.2023

Timu hiyo imecheza mechi tatu mfululizo bila ushindi katika mechi za Ligi Kuu Bara na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu ya Simba, imekutana na wachezaji kambini Mbweni nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na kujadiliana mwenendo wa timu hiyo katika mashindano mbalimbali.

Baada ya kikao hicho, wakatoka na kauli moja kwamba 'Sasa shughuli ndiyo inaanza'.

Kichapo cha mabao 5-1 walichofungwa na Yanga Novemba 5, Simba ilitoka sare ya 1-1 mara mbili mfululizo dhidi ya Namungo ya Ligi Kuu na Asec Mimosas ya Ivory Coast katika mechi ya Kundi B Ligi ya Mabingwa Afrika, ndizo zilizosababisha kuwepo kwa kikao hicho.

Kwa mujibu wa taarifa iliyowekwa katika mtandao wa klabu hiyo, ilionesha picha mbalimbali za viongozi wa klabu hiyo pamoja na wachezaji wao wakiwa katika kikao.

Baadaye ilionekana viongozi hao pamoja na wachezaji wakishikana mikono wakiwa na nyuso za furaha ikielezwa kila kitu kimewekwa sawa kwa sasa.

Mchezo ujao Simba itakuwa mgeni wa Jwaneng Galaxy Jumamosi Uwanja wa Francistown jijini Francistown nchini Botswana mechi nyingine ya Kundi B.

Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu mpya wa kikosi hicho, raia wa Algeria, Abdelhak Benchikha, anatarajia kuwasilia nchini kesho usiku akitokea nchini kwao.

Kocha huyo amekubaliana uongozi wa Simba kusaini mkataba wa mwaka mmoja na nusu ambao atamwaga wino mara moja akishafika nchini.

Uongozi wa Simba umemleta kocha huyo baada ya kuachana na aliyekuwa Kocha wao, Roberto Oliveira 'Robertinho' tangu mwanzoni mwa mwezi huu.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, inaelezwa viongozi wanahaha kuhakikisha Benchikha anakamilisha taratibu zote za kuingia nchini na ikiwezakana aweze kusafiri na timu kwenda Botswana.

Tags: