Kocha mpya Simba SC ataja mambo 3 atakayoanza nayo

LIGI KUU Kocha mpya Simba SC ataja mambo 3 atakayoanza nayo

Zahoro Mlanzi • 19:54 - 28.11.2023

Ana uzoefu wa kufundisha soka la Afrika kwa miaka 20, akipita katika timu za Raja Casablanca, Club Africain, timu ya Taifa ya Algeria, RS Berkane na CR Belouizdad.

Kocha mpya wa timu ya Simba SC, Abdelhak Benchikha, amesema ataanza na mambo matatu ndani ya timu hiyo katika kuhakikisha wanafikia malengo yao.

Mambo hayo ni kurejesha heshima ya klabu, kuongeza uzoefu na kufanya vizuri kwenye mashindano yoyoye ambayo timu inashiriki.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa utambulisho wake, Benchikha amesema amekuja katika timu ambayo anaijua na alikuwa akiifuatilia tangu zamani.

Amesema Simba ni moja kati ya timu kubwa barani Afrika na inapaswa kuheshimiwa na wapinzani hivyo yeye amekuja kutengeneza heshima hiyo ambayo kwa siku za hivi karibuni imepotea.

"Hii ni moja kati ya klabu bora barani Afrika, nimekuwa nikiifuatilia na ninajua baadhi ya vitu kuhusu hii timu, nayajua matokeo yao ya nyuma na ndio maana nipo hapa ili kujaribu kuweka mambo sawa," amesema.

Mbali na suala la kurejesha heshima lakini pia Benchikha ameahidi kuwekeza uzoefu wake katika kufundisha soka na anaamini Simba itakuwa ni timu tishio kama atapata ushirikiano kutoka kwa wachezaji, mashabiki na viongozi.

Benchikha ana uzoefu wa kufundisha soka Afrika kwa zaidi ya miaka 20. Ameshafundisha klabu mbalimbali kubwa ikiwemo Raja Casablanca, Club Africain, timu ya Taifa ya Algeria, RS Berkane na CR Belouizdad.

Mara ya mwisho kocha huyo aliipa ubingwa wa Kombe la Shirikisho timu ya USM Algerna kisha alishinda taji la Super Cup kwa kuifunga Al Ahly mwanzoni wa msimu huu.

Kocha huyo ametua nchini kuchukuwa nafasi ya Roberto Oliviera 'Robertinho' na anatarajia kuanza kibarua chake kwa mchezo wa kimataifa ambapo Simba watakabiliana na Jwaneng Galaxy ya nchini Botswana Jumamosi.

Benchikha amekuja pamoja na wasaidizi wake wawili ambao ni Farid Zemiti ambaye ni Kocha Msaidizi na Kamal Boudjenane ambaye ni Kocha wa Viungo.

Kwa upande wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Iman Kajula, amesema wameingia mkataba wa miaka miwili na kocha huyo wakiamini atafanya makubwa ndani ya klabu yao.

“Simba sio klabu ya kumpangia mwalimu mchezaji wa kumtumia, mwalimu amekuja na makocha wenzake wawili ambao ameshirikiana nao kwenye mafanikio ambayo ameyapata Afrika,” amesema.

Tags: