Kocha Simba SC aahidi kutembeza kichapo kwa wapinzani

KANDANDA Kocha Simba SC aahidi kutembeza kichapo kwa wapinzani

Na Zahoro Juma • 18:30 - 04.02.2024

Huyo ni Abdelhak Benchikha ambaye ameiongoza timu hiyo kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mashujaa FC na kufikisha alama 26 ikishika nafasi ya tatu

Kocha wa timu ya Simba SC, Abdelhak Benchikha, ametamba wataendelea kukusanya alama tatu katika mechi zao licha ya ugumu wa ratiba unaowakabili.

Hayo ameyasema ikiwa ni baada ya kuifunga Mashujaa bao 1-0 ugenini katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika Jumamosi.

Katika mchezo huo, bao la ushindi la Simba limefungwa mapema kipindi cha kwanza na Saido Ntibanzokiza aliyefunga kwa mkwaju wa penalti.

"Ratiba ni ngumu, tunacheza mechi kila baada ya siku mbili, hata hivyo hiyo haiwezi kutuzuia sisi kufanya vizuri maana tunayo timu nzuri na kikosi kipana ambacho kinaweza kupambana," amesema.

Mara baada ya mechi hiyo dhidi ya Mashujaa, Simba bado wamebakia Kanda ya Ziwa ambapo Jumanne itakuwa na mchezo mwingine muhimu dhidi ya Tabora United katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.

Simba imeanza ratiba hii ikiwa ni muendeleo wa kula viporo vyao ambavyo vililimbikizwa kutokana na ushiriki wao katika mechi za kimataifa na ratiba ya timu ya taifa ambayo ilikuwa ikishiriki Afcon.

Ndani ya siku 10 kuanzia Februari 3, Simba inalazimika kucheza takribani mechi 4 za ligi.

Ratiba inaonesha kuwa mara baada ya Simba kumalizana na Tabora United, watarejea Dar es salaam kucheza na Azam, Februari 9 kisha watasafiri kwenda Geita kuwafata Geita Gold katika mchezo ambao umepangwa Februari 12.

Tags: