Mzize aipa Yanga SC ushindi wa tano mfululizo

KANDANDA Mzize aipa Yanga SC ushindi wa tano mfululizo

Na Zahoro Mlanzi • 21:15 - 08.11.2023

Hilo ni bao lake la kwanza kufunga tangu msimu huu kuanza lakini ana asisti zaidi ya tatu

Bao pekee lililofungwa dakika ya 69 na Clement Mzize, limeiwezesha timu yake ya Yanga SC, kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union ya jijini Tanga.

Ushindi huo, umeifanya Yanga kuendelea kujichimbia kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa kufikisha alama 24 ikifuatiwa na Azam FC yenye alama 19 na Simba alama 18.

Wenyeji Coastal ambao walikuwa katika uwanja wao wa Mkwakwani, imebaki katika nafasi ya 13 kwa alama zao 7.

Yanga ambao wachezaji wake walionekana kuwa na uchovu kutokana na Jumapili iliyopita kucheza na Simba na ikashinda mabao 5-1, walipambana kupata ushindi huo.Mechi ya mwisho Yanga kufungwa alifungwa na Ihefu 2-1.

Mzize ambaye aliingia badala ya Kennedy Musonda, alifunga bao hilo pekee kwa kichwa akiunganisha mpira wa krosi uliopigwa na Jesus Moloko aliyeingia badala ya Mudathir Yahaya.

Katika kipindi cha kwanza, timu zote zilishambuliana kwa zamu huku Coastal muda mwingi ilionekana kucheza nyuma ya mpira.

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi, alifanya mabadiliko ya wachezaji watatu tofauti na kikosi kilichocheza na Simba na kuwapa nafasi kwa Kipa, Abutwalib Mshery, Nickson Kibabage na Nahodha, Bakari Mwamnyeto ambao walianza.

Baada ya Yanga kufunga bao hilo, ndipo Coastal ilionekana kushangamka na kutoka nyuma na kuanza kulishambulia lango la Yanga lakini haikusaidia kitu.

Hata hivyo hadi dakika 90 zikimalizika Yanga iliibuka na ushindi huo ukiwa na wa tano mfululizo katika ligi hiyo.

Baada ya mchezo huo Yanga sasa akili yao itahamia kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi ambapo mara baada ya mapumziko ya timu za taifa watavaana na CR Belouizdad Novemba 25.

Tags: