Yanga kuivaa APR, Simba na Jamhuri robo fainali Mapinduzi Cup

KANDANDA Yanga kuivaa APR, Simba na Jamhuri robo fainali Mapinduzi Cup

Na Zahoro Mlanzi • 09:33 - 06.01.2024

Hatua hiyo itaanza kuchezwa Jumapili na Jumatatu kwa kupigwa mechi mbili kwa siku

Hatua ya robo fainali ya michuano ya Mapinduzi Cup, inatarajiwa kuanza kesho kwa mabingwa watetezi, timu ya Mlandege FC kuumana na KVZ huku Yanga SC itacheza na APR ya Rwanda.

Robo fainali ya zingine zitachezwa Jumatatu ambapo Azam FC itaumana na Singida Fountain Gate ikifuatiwa na Simba itakayomenyana na Jamhuri FC.

Ratiba hiyo imetolewa na waandaaji wa michuano hiyo mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa Simba dhidi ya APR ambazo zilitoka suluhu katika mchezo wa mwisho wa Kundi B.

Matokeo hayo, yameifanya Simba kumaliza kinara ikiwa na alama saba kutoka kundi hilo ikifuatiwa na Singida FG yenye alama sita na APR ikishika nafasi ya tatu kwa alama zao nne.

APR imetinga hatua hiyo kutokana na kuwa ni mojawapo kati ya timu mbili zenye matokeo mazuri zaidi 'Best Loser' ukilinganisha na timu zingine zilizoshika nafasi ya tatu.

Timu nyingine iliyoingia kama 'Best Loser' ni Jamhuri FC kutoka Kundi C ambapo kundi hilo liliongozwa na Azam FC ikifuatiwa na Mlandege FC.

Mechi hizo zote za robo fainali zitapigwa kuanzia saa 10 jioni na nyingine saa 2.15 usiku kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar.

Kabla ya ratiba hiyo kutolewa, Simba imejihakikishia nafasi ya kwanza katika Kundi B kwa kutoka suluhu na APR.

Kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha katika mchezo huo ambao Simba tayari ilishakata tiketi ya robo fainali, amempa nafasi kipa, Hussein Abel ambaye alisajiliwa kutoka KMC.

Kipa huyo alijiunga tangu mwanzo wa msimu lakini hajawahi kupatiwa nafasi yoyote ya kucheza na hata alipocheza alionekana kuwa katika kiwango kizuri.

Hata hivyo, kipa huyo alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora mechi hiyo na kukabidhiwa zawadi ya Tsh500,000.

Mbali na kipa huyo, Benchikha pia alimpa nafasi mshambuliaji raia wa Zimbabwe, Michael Charamba ambaye taarifa zinadai kuwa yupo kwa majaribio kwenye klabu hiyo.

Taarifa za awali zilidai kuwa mchezaji huyo ni mali ya Simba lakini baada ya mwandishi wa mtandao huu kufatilia imethibitika kuwa mchezaji huyo yupo kwenye majaribio na atasajiliwa endapo atalifurahisha benchi la ufundi.