Simba SC katika hali tete kwenye Ligi Kuu

KANDANDA Simba SC katika hali tete kwenye Ligi Kuu

Zahoro Mlanzi • 20:30 - 09.11.2023

Timu hiyo imetoka sare ya bao 1-1 na Namungo FC ikiwa ni siku chache zimepita tangu ifungwe mabao 5-1 na watani zao wa jadi, Yanga.

Timu ya Simba SC, imeendelea kutofanya vizuri katika mechi zake za Ligi Kuu Bara baada ya kubanwa mbavu na Namungo FC kwa kutoka sare ya bao 1-1.

Huo ni mchezo wa kwanza kwa Simba tangu itoke kufungwa mabao 5-1 na Yanga SC katika mechi za ligi hiyo.

Mchezo huo ulipigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, umeifanya timu hiyo kuvuna alama 1 na kufikisha alama 19 sawa na Azam FC ila inabaki katika nafasi ya tatu kwa kutokuwa na uwiano mzuri wa mabao na Namungo ikibaki nafasi ya 10 kwa alama zao 8. Yanga inaongoza ligi hiyo ikiwa na alama 21.

Namungo ndio ilikuwa ya kwanza kufunga bao dakika dakika ya 28 kupitia kwa straika wao, Reliants Lusajo aliyepiga shuti akiwa ndani ya eneo la hatari na mpira kujaa wavuni huku kipa, Lakred Ayoub akiruka bila mafanikio.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Namungo ilikuwa mbele kwa bao 1-0 licha ya Simba kuonekana kutawala mchezo muda mwingi na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga.

Moja ya nafasi ambazo itajutia ni aliyopata Jean Baleke ambaye alishindwa kuunganisha krosi iliyopigwa na Mohamed Hussein na mpira kutoka nje.

Kipindi cha pili, Namungo iliendelea kucheza mfumo wao wa kuwa nyuma ya mpira lakini mabadiliko yaliyofanywa na Kocha wao, Denis Kitambi kwa kuwatoa baadhi ya wachezaji kama Frank Domayo na Pius Buswita ambao walionekana kucheza vizuri eneo la katikati ndipo ikaleta utofauti.

Simba ilisawazisha bao hilo dakika ya 75 kupitia kwa Baleke ambaye hilo ni bao lake la saba msimu huu, akiunganisha krosi ya Mosses Phiri aliyeingia badala ya Andre Onana.

Baada ya kufunga bao hilo, Simba iliendelea kuipa presha Namungo lakini timu hiyo inayotoka Kusini mwa Tanzania, ilikuwa imara katika kuzuia na kuondoa hatari zote golini mwao.

Simba kwa sasa haitakuwa na mchezo wowote hadi pale timu za Taifa zitakapomaliza mechi zao za kuwania kufuzu Kombe la Dunia.

Tags: