Yanga SC yabanwa mbavu na Kagera ugenini

Kiungo wa timu ya Yanga SC, Mganda Khalid Aucho (kulia), akitafuta njia ya kumtoka straika wa Kagera Sugar, Obrey Chirwa

LIGI KUU Yanga SC yabanwa mbavu na Kagera ugenini

Na Zahoro Juma • 20:48 - 02.02.2024

Matokeo hayo yameifanya timu hiyo kubaki nafasi ya pili nyuma ya Azam FC

Klabu ya Soka ya Yanga, imeshindwa kukwea kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kulazimishwa suluhu na Kagera Sugar kwenye mchezo ambao umefanyika Uwanja wa Kaitaba, mkoani Kagera.

Alama tatu kwa Yanga zingetosha kuwapandisha juu ya msimamo wakifikisha alama 34 na kuwashusha Azam ambao wangebaki na alama 33.

Kwa matokeo hayo, sasa wataendelea kubakia katika nafasi ya pili wakifikisha jumla ya alama 32 baada ya kushuka dimbani mara 12.

Yanga ambao waliingia na uchu wa kupata alama tatu, ilijikuta katika wakati mgumu kupasua ngome ya Kagera Sugar iliyokuwa chini ya ulinzi wa nahodha, Abdallah Mfuko.

Kwa dakika zote 90, Kagera walicheza kwa nidhamu ya ulinzi huku pia Kipa wao, Ramadhan Chalamanda akifanya kazi ya ziada kuokoa michomo hatari.

Nafasi kubwa kwa Yanga kufunga bao zilipatikana kipindi cha pili ambapo Pacome Zouzoua alishindwa kuunganisha golini krosi kutoka kwa Nickson Kibabage.

Pia Kennedy Musonda ambaye aliingia kipindi cha pili alishuhudia jaribio lake la kichwa likiokolewa na kipa Charamanda.

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi, alimuingiza kikosini mshambuliaji wake mpya, Joseph Guede, hata hivyo hakuweza kuonesha cheche zake kutokana na uimara wa safu ya ulinzi ya Kagera Sugar.

Mara baada ya mchezo huo Yanga, inarejea Dar es Salaam kwa ajili ya kuwakabili Dodoma Jiji katika mchezo ambao utapigwa Jumatatu.

Tags: