Yanga SC kuongeza 'mashine' mpya dirisha dogo

LIGI KUU Yanga SC kuongeza 'mashine' mpya dirisha dogo

Na Zahoro Mlanzi • 22:00 - 09.11.2023

Uongozi hauna shida kuhusu kutekeleza mahitaji ya kocha, ripoti ya kocha kama itaonesha kuna uhitaji wa wachezaji, sisi tutatekeleza

Rais wa Klabu ya Yanga SC, Injinia Hersi Said, amesema licha ya kuwa timu yao inafanya vizuri kwasasa lakini bado wana mpango wa kufanya maboresho kwenye dirisha la usajili mwezi ujao.

Dirisha la usajili linatarajiwa kufunguliwa Desemba 15 na timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu na hata madaraja ya chini zitakuwa na nafasi ya kuongeza wachezaji.

Akizungumza na Pulsesports, Injinia Hersi, amesema bado kuna nafasi ndani ya kikosi ambazo zinahitaji maboresho na hiyo ni kwa mujibu wa Kocha, Miguel Gamond.

Amesema wao kama uongozi hawana shida na kwamba wanachotaka kutekeleza ni matakwa ya kocha tu na si kingine.

Yanga wanaongoza ligi wakiwa na alama 24 mbele ya Azam wenye alama 19 sawa na Simba SC ila zinatofautiana kwa mabao.

Mbali na michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara lakini Yanga wanashiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika ambapo kwasasa wapo kwenye hatua ya makundi na mechi hizo zinatarajia kuanza mwishoni mwa mwezi huu.

Yanga wamepangwa kwenye kundi moja na timu za Al Ahly, Medeama na CR Belouizdad na kwamba wataanzia ugenini Novemba 25 kuumana na Belouizdad ya Algeria.

Baadhi ya maoni yamekuwa yakielekezwa kuwa pengine Yanga hawakuziba vizuri nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mshambuliaji wao, Fiston Mayele aliyetimkia Pyramids ya Misri mwanzoni mwa msimu huu.

Mchezaji ambaye alisajiliwa moja kwa moja kwa ajili ya kuziba nafasi ya Mayele alikuwa ni Mghana, Hafidh Konkoni ambaye hadi sasa inaonekana kuwa haaminiki kwa Kocha Gamondi.

Katika dirisha lililopita la usajili, Yanga waliwasajili Pacome Zouazoa, Max Nzengeli, Yao Kouassi, Makudubela Mahlatse 'Skudu', Gift Fred, Nickson Kibabage, Konkoni na Jonas Mkude.

Tags: