Kocha Twiga Stars aihofia Botswana kufuzu Olimpiki

© Kwa Hisani

KANDANDA Kocha Twiga Stars aihofia Botswana kufuzu Olimpiki

Zahoro Mlanzi • 11:04 - 31.10.2023

Timu hizo zinatarajiwa kurudiana kesho katika mchezo wa kuwania kufuzu Olimpiki ya Paris 2024 ambapo katika mechi ya kwanza Twiga Stars ilishinda 2-0.

Kocha wa timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania 'Twiga Stars', Bakari Shime, amesema mchezo wao wa marudiano dhidi ya Botswana utakuwa mgumu kutokana na wapinzani wao bado wanataka matokeo mazuri.

Timu hizo zinatarajiwa kurudiana kesho katika mchezo wa kuwania kufuzu Olimpiki ya Paris 2024 ambapo katika mechi ya kwanza Twiga Stars ilishinda 2-0 uwanjani Azam Complex, Dar es Salaam.

Kwa matokeo hayo, Twiga Stars wanahitajika kupata sare au kutoruhusu mabao ya zaidi ya mawili ili kusonga mbele hatua inayofuata.

Mshindi wa jumla kati ya Twiga Stars na Botswana anatarajia kukutana na DRC au Afrika Kusini katika mechi ya mzunguko wa tatu iliyopangwa kuchezwa Februari, mwakani.

Akizungumzia maandalizi kuelekea mechi hiyo, Kocha Shime, amesema vijana wake wamejiandaa vizuri na wapo tayari kwa mchezo huo muhimu.

Amesema mchezo huo unatarajiwa kuwa mgumu kwa upande wao kwasababu wapinzani wao bado hawajakata tamaa wana matumaini ya kusonga mbele hivyo wataingia uwanjani kwa lengo la kupambana.

"Maandalizi tumeyafanya vizuri lakini bado tunatakiwa kupambana ili kuwaondoa wapinzani wetu, matokeo ya kupoteza 2-0 hayakuwakatisha tamaa hivyo bado wana hali ya kutaka matokeo," amesema.

Katika mchezo uliofanyika Dar es Salaam, mabao ya Twiga Stars yalifungwa na Oppa Clement na Aisha Masaka.