Aziz KI, Job, Nzengeli wawania Tuzo Mchezaji Bora Yanga

© Kwa Hisani

KANDANDA Aziz KI, Job, Nzengeli wawania Tuzo Mchezaji Bora Yanga

Zahoro Mlanzi • 21:09 - 28.10.2023

Aziz KI ameingia kuwania tuzo hiyo akiwa ametoka kufunga mabao matatu 'Hat trick' dhidi ya Azam huku Nzengeli akiwa ametoka kufunga mabao mawili dhidi ya Singida Fountain Gate.

Majina ya nyota watatu wa timu ya Yanga SC, yamepenya kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa mwezi ndani ya timu hiyo.

Yanga hivi karibuni iliingia ushirikiano na NIC kwa ajili ya kutoa zawadi kwa wachezaji wa timu hiyo watakaofanya vizuri ndani ya mwezi husika.

Mwezi huu vinara hao wa Ligi Kuu Bara wakiwa na pointi 18 baada ya kucheza mechi saba za ligi hiyo, wameanza mchakato wao wa kumsaka mchezaji bora wa mwezi.

Kwa mujibu wa Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Yanga, Ali Kamwe amesema kura zitapigwa na mashabiki kupitia Yanga App.

“Majina matatu ambayo kamati imeyaleta kwa uongozi wa Yanga kuwania tuzo ya mchezaji bora wa mwezi ni Stephane Aziz Ki, Dickson Job pamoja na Max Nzengeli, majina haya yatapigiwa kura kupitia Yanga APP”.

Aziz KI ameingia kuwania tuzo hiyo akiwa ametoka kufunga mabao matatu 'Hat trick' dhidi ya Azam huku Nzengeli akiwa ametoka kufunga mabao mawili dhidi ya Singida Fountain Gate.

Wakati Job yeye ni kutokana na kazi kubwa ya ulinzi aliyofanya katika michezo hiyo miwili mikubwa pamoja na iliyotangulia.

Timu hiyo kwa sasa inajiandaa na mchezo wao wa Novemba 5 dhidi ya mahasimu wao, Simba SC.