Gamondi 'anasa' faili la Simba SC

Ligi Kuu: Gamondi 'anasa' faili la Simba SC

Na Zahoro Mlanzi • 19:00 - 29.10.2023

Hii itakuwa ni 'Derby' ya pili kwa Gamondi.

Hili limekwisha! Unaweza kusema hivyo baada ya Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi, 'kulinasa faili' la Simba kabla ya kukutana nao mwishoni mwa wiki kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara.

Kocha huyo raia wa Argentina, alikuwa jukwaani kuwatazama Simba wakati wakicheza na Ihefu FC kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Amefika uwanjani hapo akiongozana na Meneja wa Yanga, Walter Harrison, mapema dakika 40 kabla ya kuanza kwa mchezo na aliangalia mazoezi ya viungo 'warm up' kabla ya mchezo.

Muda mwingi wa mazoezi hayo, Gamondi ameonekana kuwa makini kufuatilia kila hatua na mara kadhaa alionekana akinong'ona na Harrison.

Hata wakati wa mechi ilipoanza Gamondi amekuwa makini zaidi na wakati mwingine akiandika baadhi ya vitu katika kitabu kidogo alichokwenda nacho.

Katika mchezo huo, Simba wameshinda mabao 2-1 huku mabao kwa upande wa Simba yakifungwa na Jean Baleke na Moses Phiri.

Mara baada ya mchezo huo, Gamondi alikataa kuzungumza lolote huku Harrison akimsindikiza hadi katika eneo la maegesho ya magari.

Ikumbukwe Jumapili miamba ya soka la Tanzania, Simba watawakaribisha Yanga kwenye mchezo wa ligi hiyo mzunguko wa nane.

Hadi sasa Yanga ipo kileleni wakiwa na alama 18 sawa na Simba ambao wana mchezo mmoja mkononi.

Hii itakuwa ni 'Derby' ya pili kwa Gamondi. Alikutana na Simba kwa mara ya kwanza kwenye fainali ya Ngao ya Jamii ambapo alipoteza mchezo huo kwa mikwaju ya penalti baada ya dakika 90 kutoka suluhu.

Tags: