Taifa Stars yaahidi kupambana ikiivaa Morocco leo AFCON

Kikosi cha Taifa Stars, kilichocheza na Misri mchezo wa kirafiki mapema mwezi huu

KANDANDA Taifa Stars yaahidi kupambana ikiivaa Morocco leo AFCON

Zahoro Juma • 09:30 - 17.01.2024

Taifa Stars inashiriki michuano hiyo kwa mara tatu katika historia yao

Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', leo saa 2 usiku kwa saa za Afrika Mashariki na Kati, kitashuka uwanjani kuumana na Morocco katika mfululizo wa mechi za michuano ya AFCON inayoendelea nchini Ivory Coast.

Stars ambayo imepangwa Kundi F, itaumana pia na timu za Zambia na DR Congo katika kuwania kutinga robo fainali ya michuano hiyo.

Mchezo huo utapigwa katika Uwanja wa Laurent Pokou uliopo katika Mji wa San Pedro.

Taifa Stars inakutana na Morocco kwa mara ya kwanza katika historia ya michuano hiyo.

Awali timu hizo zimeshawahi kukutana katika mechi tano za michuano ya kufuzu ambapo Morocco wanarekodi ya kushinda michezo minne huku Stars wakishinda mchezo mmoja.

Mechi ya mwisho kukutana kwa wawili hao ilikuwa ni Novemba 21, mwaka jana kwenye mchezo wa kufuzu kuwania Kombe la Dunia ambapo Morocco walishinda mabao 2-0, mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.

Stars inashiriki michuano hiyo kwa mara ya tatu katika historia yao ikiwa pia waliwahi kushiriki mwaka 1980 nchini Nigeria na mwaka 2019 nchini Misri.

Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Kocha wa Stars, Adel Amrouche, amesema timu ipo kamili na wamepata muda wa kutosha kujiandaa hivyo wanatarajia kuwa na mchezo mzuri.

"Maandalizi yetu tumeyafanya kwa ubora ambao tuliokusudia kwa asilimia kubwa, tunaamini tunaweza kutoa mchezo mzuri dhidi ya Morocco na tutapambana kwa hali na mali," amesema.

Katika kikosi cha Stars kimeongezewa nguvu na nyota wanaocheza England kama Haji Mnoga anayekipiga Aldershot Town's, Tarryn Allarakhia wa Weildstone FC pamoja na Ben Starkie wa Ilkestone Town's.

Kocha Amrouche atakuwa na kazi ya ziada ya kupanga kikosi chake kwani wachezaji 23 aliowaita kila mmoja amekuwa akionesha ubora wake hususani kama ilivyokuwa katika mechi ya mwisho ya kirafiki dhidi ya Misri ambayo Stars ilifungwa 2-0.

Pamoja na hilo lakini Amrouche anatarajiwa golini leo kuanza na Kipa, Aishi Manuala akisaidiwa na mabeki Starkie, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Abdullah 'Bacca', Mohamed Hussein 'Tshabalala' na viungo ni Sospeter Bajana, Novatus Dismas na Feisal Salum 'Fei Toto' wakati washambuliaji ni Simon Msuva, Mbwana Samatta na Allarakhia.

Tags: