Yanga SC yajichimbia kileleni Ligi Kuu

Mchezaji wa Yanga, Pacome Zouzoua (kulia), akishangilia na wenzake

KANDANDA Yanga SC yajichimbia kileleni Ligi Kuu

Na Zahoro Juma • 18:49 - 17.02.2024

Ni baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 mbele ya KMC na kufikisha alama 43

Vinara wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara, timu ya Yanga, imeendeleza vicheko juu ya msimamo wa ligi baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya KMC.

Mchezo huo wa kwanza wa raundi ya pili kwa kila timu umechezwa katika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Mchezaji ambaye yupo kwenye kiwango bora kwasasa, Mudathir Yahaya ndiye alifunga mabao mawili katika mchezo huo huku bao la kwanza akifunga dakika ya kwanza tu ya mchezo.

Mabao hayo yanamfanya Mudathir kuwa amefunga mabao matatu katika mechi tano za ligi tangu iliporejea huku pia akifikisha mabao sita kwenye msimu hadi sasa.

Bao lingine la Yanga lilifungwa na Pacome Zouzoua ambaye alifunga pia katika mchezo uliopita, na sasa anakuwa amefikisha mabao sita kwenye msimu wa ligi hii.

Yanga ingeweza kufunga mabao mengi zaidi hasa kipindi cha kwanza lakini Clement Mzize alionekana kukosa utulivu kwenye nafasi nyingi alizotengenezewa.

Kipindi cha pili, Kocha Miguel Gamondi alimtoa Mzize na kumpa nafasi mshambuliaji Joseph Guede ambaye naye alikosa mabao mawili moja akigongesha mwamba na nafasi nyingine ikiokolewa na Kipa, Denis Richard.

Kwa ushindi huo, Yanga imefikisha alama 43 ambazo ni saba zaidi ya Simba waliokuwa kwenye nafasi ya pili lakini wana faida ya mchezo mmoja mkononi.