Yanga SC yazindua kadi ya uanachama yenye thamani ya sh. milioni 1

Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, akikabidhiwa kadi hiyo na Mkurugenzi wa Biashara wa NMB, Filbert Mponzi

KANDANDA Yanga SC yazindua kadi ya uanachama yenye thamani ya sh. milioni 1

Na Zahoro Juma • 16:20 - 08.02.2024

Kadi hiyo itamnufaisha mwanachama katika masuala mbalimbali zikiwemo huduma za kijamii na kibenki

Klabu ya soka ya Yanga, imezindua kadi mpya za wanachama yenye gharama ya shilingi milioni moja.

Kadi hiyo imezinduliwa kwa ushirikiano na Benki ya NMB na itakuwa inajulikana kwa jina la 'Black Card'.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam, Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, amesema zoezi la uzinduzi wa kadi hiyo ni muendelezo wa shamra shamra kueleka miaka 89 ya tangu kuanzishwa kwa timu hiyo kongwe nchini.

Amesema wanachama watakaoweza kukata kadi hiyo watanufaika kwa huduma mbalimbali za kibenki na kijamii lakini hata kwa upande wa klabu ambayo wanaishangilia.

"Kadi hii kutokana na umuhimu wake tumeona tuweke na baadhi ya ofa za kuvutia ambazo zitakuwa ni faida kwa mwanachama mwenye kadi hii," amesema.

Kwa upande wa faida za kitimu, Hersi amesema mwanachama mwenye kadi hiyo atakuwa na uhakika wa kupewa tiketi 10 za jukwaa maalumu 'VIP' kwa mechi ambazo Yanga watakuwa katika uwanja wa nyumbani.

Mbali na faida hiyo lakini pia mwanachama huyo atajihakikisha seti sita za jezi mpya kila msimu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, amezitaja faida za kibenki ambazo mwanachama atanufaika nazo kuwa ni pamoja na mikopo ya hapo kwa hapo.

Mbali na mikopo lakini mwanachama mwenye kadi hiyo atanufaika na huduma mbalimbali na ofa ambazo mara kadhaa hutolewa na Benki ya NMB.

Yanga inatarajia kutimiza miaka 89 tangu kuanzishwa kwao Februari 11 ambapo tayari walishatangaza kuwa sherehe zao kitaifa zitafanyika mkoani Mbeya ambapo pia siku hiyo watakuwa na mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Tanzania Prisons.

Tags: