Kocha Azam FC aponda kiwango cha Simba SC

KANDANDA Kocha Azam FC aponda kiwango cha Simba SC

Zahoro Juma • 15:32 - 10.02.2024

Kauli hiyo imetolewa na Kocha Mkuu, Yusuph Dabo baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1

Kocha wa timu ya Azam FC, Yusuph Dabo, amesema Simba hawakucheza mpira wowote zaidi ya 'butua butua' na anajilaumu kwa kutoweza kupata ushindi kwenye mchezo wao wa Ligi Kuu Bara ambao uliisha kwa sare ya 1-1.

Mchezo huo ulifanyika Jana Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza ambapo ulishuhudiwa Azam wakipata bao la mapema kipindi cha kwanza kupitia kwa Prince Dude lakini Simba wakachomoa dakika za mwishoni kupitia kwa Clotus Chama.

"Simba hawakuwa na mpango wowote mzuri zaidi ya mipira mirefu, tuliweza kutekeleza mbinu zetu kwa nidhamu ya hali ya juu lakini bahati mbaya matokeo hayajawa upande wetu," amesema.

Mbali na hilo lakini Dabo pia alizikumbuka nafasi za wazi walizopoteza kwenye mchezo huo huku akisema kama wangekuwa makini wangeweza kupata ushindi tangu kipindi cha kwanza.

Amesema waliiheshemu Simba kwasababu ya historia ya ukubwa wao lakini kwasasa uwanjani hata timu yake ya Azam inapaswa kupewa heshima.

Simba na Azam imekuwa ni moja kati ya mechi zenye mvuto kwa siku za hivi karibuni kutokana na ushindani ambao umeongezeka baina yao.

Katika mechi mbili za ligi ambazo zilifanyika msimu uliopita, Azam waliibuka na ushindi katika mechi moja na huku nyingine ikiisha kwa sare.